TFF.
Shirikisho la soka nchini TFF
limesimamia msimamo wake wa kuheshimu ratiba ya kuanza kwa msimu mpya wa
2018/17, licha ya kushauriwa kurudisha nyuma mchezo wa kuwani ngao ya jamii
ambao utawakutanisha mahasimu wa soka la Bongo Wekundu wa Msimbazi Simba dhidi
ya Young Africans.
Afisa habari wa shirikisho hilo
Alfred Lucas amesema wanaheshimu mawazo na michango iliyowasilishwa TFF na
wadau wa soka kuhusu mabadiliko ya mchezo huo, lakini akaeleza hawatobadilisha
tarehe ambayo waliitangaza wakati wakitoa ratiba ya msimu mpya.
Zoezi la kuchukua fomu za kuwani
nafasi za uongozi wa kamati ya bodi ya ligi zimeanza kwa kusuasua ikiwa ni siku
ya kwanza ya mchakato wa kuelekea kwenye uchaguzi ambao utafanyika jijini Dar
es salaam mwezi ujao.
Afisa habari wa shirikisho la soka
nchini TFF Alfred Lucas amesema waliutarajia huenda viongozi wa klabu za ligi
kuu na ligi daraja la kwanza wangejitokeza kwa wingi hii leo, lekini imekua
tofauti.
Wakati huo huo wachezaji watatu
waliokuwa kwenye timu ya soka ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17,
Serengeti Boys, Ally Ng’anzi, Yohana Oscar Nkomola na Erick Nkosi wameondoka
nchini Alfajiri ya leo kwenda Tunisia kwa ajili ya majaribio ya kucheza soka ya
kulipwa.
Serengeti Boys ikiundwa na vijana wenye vipaji kutoka
mikoa tofauti, iliweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza ya vijana Tanzania kucheza
Fainali za Afrika baada ya kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana chini
ya umri wa miaka 17 mwezi Mei mwaka huu nchini Gabon.
Na kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa Cambiasso Sports
Centre, Twaha Ngwambi, vijana hao wote wamepata mwaliko wa klabu ya Etoile du
Sahel ya Ligi Kuu ya Tunisia.
Ngwambia amesema mwaliko huo unafuatia vijana hao wote
kufanya vizuri wakiwa na timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17
mwaka huu.
Ngwambia amesema kwamba Ng’anzi na Nkosi wanakwenda
kufanya majaribio, wakati Nkomola anakwenda moja kwa moja kujiunga na akademy
ya timu hiyo ambako atasaini mkataba.
Pamoja na kutolewa katika hatua ya makundi nchini Gabon,
Serengeti Boys ilivutia kwa soka yake, huku vijana wengi wakitabiriwa kufika
mbali zaidi kisoka.

No comments
Post a Comment