Na Emason Kadig. Balohafmtz Blog.
JUVENTUS YAMUULIZIA CAHILL

Juventus inaangalia uwezekano wa kumsajili beki wa Chelsea na timu ya Uingereza Gary Cahill, kwa mujibu wa The Sun .
Mabingwa hao wa Serie A wameulizia upatikanaji wa beki huyo wa kati wakiwa wanatafuta mrithi wa Leonardo Bonucc, ambaye ametimkia AC Milan, Chelsea nao wametajwa kuwa kwenye mchakato wa kutaka kumsajili Virgil van Dijk, na ujio wake utafungua njia kwa Cahill kwenda Juventus.
DRAXLER ASHINIKIZA KUONDOKA PSG
Muda wa Julian Draxler katika klabu ya PSG unakaribia ukingoni kwani mwakilishi wa mchezaji huyo yupo kwenye mazungumzo na Bayern Munich, L'Equipe limeripoti.
Mchezaji huyo alitakiwa kutimkia Monaco kama sehemu ya dili la Kylian Mbappe lakini alikataa fursa hiyo.
Barcelona pia wanamtaka mchezaji huyo wa kimataifa wa Ujerumani.
BABA MESSI AFANYA MAZUNGUMZO NA MAN CITY
Baba mzazi wa Lionel Messi, Jorge ameanza mazungumzo na Manchester City katika harakati za nyota huyo wa Barcelona kutua Uingereza 2018, kwa mujibu wa Sun .
Lionel Messi asiposaini mkataba mpya, msimu ujao anaweza kuondoka kama mchezaji huru, na Man City inaonekana kuwa karibu na wawakilishi wa mchezaji huyo.
JUVE YAUNGANA NA LIVERPOOL KUMUWINDA HOWEDES
Juventus inataka kuingia vitani dhidi ya Liverpool kuiwania saini ya beki wa Schalke, Benedikt Howedes, kwa mujibu wa habari kutoka Bild .
Jurgen Klopp anataka kumsajili Mjerumani mwenzake kuimarisha safu ya ulinzi ya Liverpool lakini pia anatamani kumpata Leonardo Bonucci.
HAZARD KUSHINIKIZA KWENDA MADRID
Nyota wa Chelsea Eden Hazard yupo tayari kufanya kila anachoweza kushinikiza uhamisho kwenda Real Madrid majira ya joto, kwa mujibu wa Don Balon .
WILLIAN KUMRITHI NEYMAR BARCELONA?
Winga wa Chelsea Willian yupo katika nafasi nzuri zaidi kutua Barcelona kurithi nafasi ya Neymar aliyetimkia PSG, kwa mujibu wa France Football .
Mbrazili huyo amekuwa na wakati mgumu kuzoea mfumo wa Antonio Conte, na amekuwa akisugua benchi kwa muda mrefu tangu ujio wa Muitaliano huyo.
GORETZKA ATOLEWA KWA BARCELONA
Schalke imemtoa kiungo wao mahiri Leon Goretzka kwa Barcelona ili kuepuka mchezaji huyo kuondoka bure msimu ujao kujiunga na mahasimu wao wa Bundesliga, Bayern Munich, kwa mujibu wa habari kutoka Mundo Deportivo .
BARCA YAKUBALI KUTOA €50M KUMSAJILI DI MARIA
Barcelona imekubali kutoa ada ya €50 millioni kumsajili Angel Di Maria kutoka Paris Saint-Germain na pia wamefikia makubaliano binafsi na mchezaji huyo wa zamani wa Real Madrid, kwa mujibu wa Sport .
BARCELONA YAMFUATILIA KEITA
Barcelona wanamfuatilia kiungo wa RB Leipzig Naby Keita klabu hiyo inapokomaa kutafuta wachezaji wa kusajili kabla ya kufungwa dirisha la uhamisho wa majira ya joto, limeripoti Mundo Deportivo .
SPURS YAKARIBIA KUMSAJILI AURIER KWA €25M
Tottenham wapo karibu kukubali ada ya euro milioni 25 kumsajili Serge Aurier kutoka Paris Saint-Germain, kwa mujibu wa L'Equipe .
Aurier amekuwa shabaha ya Chelsea na Manchester United, lakini Spurs sasa wanaonekana kuwa katika nafasi nzuri zaidi kumsajili beki huyo wa kulia baada ya kufikia makubaliano binafsi.
LILLE YATOA OFA YA €40M KWA AJILI YA BATSHUAYI
Lille wapo tayari kutoa ofa ya €40 millioni kumrejesha mshambuliaji wa Chelsea Michy Batshuayi kwenye Ligi ya Ufaransa, Ligue 1, kwa mujibu wa France Football .
KOVACIC AKUBALI KUTUA LIVERPOOL
Kiungo wa Real Madrid Mateo Kovacic amefikia makubaliano kwa maneno kujiunga na Liverpool, kwa mujibu wa Diario Gol via Daily Mirror .
Reds wameshafanya mazungumzo na mchezaji huyo wa kimataifa wa Croatia kuhusu kutua Anfield, na anatarajiwa kuziba pengo la Philippe Coutinho ikiwa atatimkia Barcelona.
CHELSEA KUTOA £91M KUMSAJILI BELOTTI
Chelsea wanaandaa kitita cha paundi milioni 91 kwa ajili ya mshambuliaji wa Torino, Andrea Belotti katika harakati zao za kutafuta mshambuliaji mwingine, kwa mujibu wa habari kutoka TransferMarketWeb .
Antonio Conte amedhamiria kuleta mshambuliaji mwingine kwenye kikosi chake kabla ya kufungwa dirisha la usajili licha ya kumsajili Alvaro Morata kutoka Real Madrid kwa paundi milioni 70.
JUVENTUS NA MAN UTD ZAMWANIA KIUNGO WA ARSENAL
Manchester United imeingia katika kinyang'anyiro cha kuiwania saini ya kiungo wa Arsenal anayekuja kwa kasi Marcus McGuane, lakini Juventus wanaongoza mbio za kumwania kinda huyo, kwa mujibu wa Independent .
SPURS YAANDAA £20M KWA AJILI YA BARKLEY
Tottenham itatoa ofa ya paundi milioni 20 kwa ajili ya kiungo wa Everton Ross Barkley, lakini wanapata ushindani kutoka kwa mahasimu wao Chelsea, kwa mujibu wa Telegraph .
MAN CITY YAGEUZIA RADA YAO KWA GIBSON MWENYE THAMANI YA £20M
Manchester City wapo tayari kuacha kumfuatilia Jonny Evens na kumgeukia beki wa Middlesbrough Ben Gibson, kwa mujibu wa The Independent .
MARCHISIO ANATAKA KUONDOKA JUVE
Claudio Marchisio anataka kuondoka Juventus kabla ya kufungwa dirisha la uhamisho wa majira ya joto, Chelsea ndiyo klabu anayotarajiwa kujiunga nayo, kwa mujibu wa Corriere della Sera .
Habari zinadai kuwa kiungo huyo hana mahusiano mema na bosi wa Juve Massimilliano Allegri na anahitaji timu itakayompa zaidi nafasi kikosi cha kwanza ili aweze kufikiriwa kwenye kikosi cha Italia Kombe la Dunia mwakani.
COUTINHO KWENDA BARCA HAIWEZEKANI
Philippe Coutinho sasa haiwezekani kujiunga na Barcelona akitokea Liverpool msimu huu wa majira ya joto kwa mujibu wa RAC1 kupitia Mundo Deportivo .
Madau kadhaa ya Barcelona kwa ajili ya mchezaji huyo yamekataliwa na klabu ya Liverpool imesisitiza Mbrazili huyo hauzwi.
PEREIRA MBIONI KWENDA VALENCIA
Valencia wanakaribia kumsajili kwa mkataba wa mkopo kiungo wa Manchester United Andreas Pereira, kwa mujibu wa Cadena Ser Valencia .
Pereira alikuwa Granada msimu uliopita na yupo mbioni kurudi kwenye La Liga msimu huu tena.
SERI AKUBALI AKUBALI KUTUA BARCA MIAKA MINNE
Kiungo wa Nice Jean-Michael Seri amefikia makubaliano ya mkataba wa miaka minne kujiunga na Barcelona, kwa mujibu wa L'Equipe.
BAYERN WAFIKIRIA KUMSAJILI DRAXLER
Bayern Munich wanaangalia uwezekan wa kumsajili mshambuliaji wa Paris Saint-Germain Julian Draxler, kwa mujibu wa Westdeutsche Allgemeine Zeitung .
Mustakabali wa Drazxler PSG haueleweki kufuatia usajili wa Neymar, na Mjerumani huyo amehusishwana tetesi za kutaka kutua Arsenal, Liverpool na Manchester United.
ARSENAL WAMPA OX MKATABA MPYA
Arsenal wamempa mkataba mpya wa miaka minne Alex Oxlade-Chamberlain wenye thamani ya paundi 125,000 kwa wiki kumzuia kwenda Chelsea, kwa mujibu wa Daily Star .
MBAPPE AACHWA MAZOEZI YA MONACO
Kylian Mbappe ameachwa kwenye mazoezi ya Monaco baada ya kufanya mabishano na Andrea Raggi Jumanne iliyopita kwa mujibu wa L'Equipe .
WILSHERE ATOLEWA KWA AC MILAN
Arsenal wamemtoa Jack Wilshere kwa AC Mila, limeripoti Corriere dello Sport .
Wilshere amehusishwa na tetesi za kujiunga na klabu hiyo ya Serie A siku za nyuma, lakini mchezaji huyo anasita kuondoka Ligi Kuu Uingereza.
MAN CITY KUTOA £70M KUMSAJILI ALEXIS
Manchester City itaendelea kumfukuzia Alexis Sanchez hadi mwisho wa dirisha la uhamisho, na wameandaa kitita cha paundi milioni 70 kwa ajili ya nyota huyo wa Arsenal, limeripoti Mirror .
CHELSEA YATENGA £200M KWA USAJILI
Chelsea wanajipanga kutumia paundi milioni 200 kusajili wachezaji wapya watano ili kutimiza anachokitaka Antonio Conte, kwa mujibu wa Express .
Wachezaji watatu wa Southampton Virgil van Dijk, Cedric Soares na Ryan Bertrand wapo kwenye orodha ya wachezaji anaowataka Conte, kadhalika Danny Drinkwater wa Leicester City na kiungo wa Arsenal Alex Oxlade-Chamberlain.
MAN UTD, ARSENAL & LIVERPOOL ZAMWANIA DRAXLER
Nyota wa Paris Saint-Germain Julian Draxler anawaniwa na klabu za Uingereza, Man United, Arsenal na Liverpool ikiwa ataondoka Parc des Princes, kwa mujibu wa Mirror .
ATLETICO YAKUBALI OFA YA €55M KWA AJILI YA COSTA
Atletico Madrid imekubali kuilipa Chelsea €55 millioni kwa ajili ya kumnunua Diego Costa, kwa mujibu wa habari.
Costa kwa sasa yupo Brazili baada ya kukataa kurejea Chelsea na klabu pekee anayoitaka kujiunga nayo kwa sasa ni Atletico Madrid.
BARCA KUFANYA MAZUNGUMZO YA MWISHO NA COUTINHO
Liverpool wamekubali kufanya mkutano wa mwisho na Barcelona kuhusu uhamisho wa Philippe Coutinho, kwa mujibu wa Sport .
Klabu hiyo ya Ligi Kuu Uingereza imekataa ofa tele kwa ajili ya mchezaji huyo, ofa ya mwisho ilikuwa euro milioni 125.
PSG MBIONI KUMTANGAZA MBAPPE
PSG wapo mbioni kutangaza usajili wa Kylian Mbappe kutoka Monaco, kwa mujibu wa habari kutoka Mundo Deportivo .
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 19 atakuwa mchezaji wa pili ghali zaidi katika historia, baada ya klabu hiyo ya Paris kumsajili Neymar kwa euro milioni 222.
€500M NDIYO BEI YA ASENSIO
Real Madrid inataka kumtunuku Marco Asensio mkataba mpya hadi 2023 na kuiongeza bei yake hadi euro mlioni 500, kwa mujibu wa Marca .
BARCA YATOA €30M KWA AJILI YA SERI
Barcelona wametoa ofa ya euro milioni 30 kwa ajili ya kiungo wa Nice Jean Michael Seri katika harakati zao za kutafuta wachezaji wapya, limedai Sport.
MADRID YAKATAA OFA YA €75M KWA KOVACIC
Real Madrid imekataa ofa ya euro milioni 75 kwa ajili ya Mateo Kovacic kutoka Juventus, kwa mujibu wa AS .
WEST BROM YAMFUKUZIA SAKHO
West Brom wanafikiria kumsajli beki wa Liverpool Mamadou Sakho baada ya Manchester City kuonesha nia ya kumsajili Jonny Evans, kwa mujibu wa BBC .
Sakho anakadiriwa kuwa na thamani ya £30 millioni na Liverpool na aling'ara alipokuwa akitumika kwa mkopo Crystal Palace msimu uliopita baada ya kukataa kujiunga na West Brom.
MADRID WAMTENGEA DE GEA DAU LA £46M
Real Madrid wanajipanga kutoa dau la paundi milioni 46 kwa ajili ya kipa nambari moja wa Manchester United, David De Gea kwa mujibu wa The Sun .
INTER YAMTIA KWENYE RADA MUSTAFI
Inter imefanya jaribio la kumsajili beki wa Arsenal Shkodran Mustafi kwa uhamisho wa mkopo, kwa mujibu wa GIanlucaDiMarzio.com .
Miamba hao wa Serie A wanataka kuimarisha safu yao ya ulinzi na wanaamini Mjerumani huyo atakuwa suluhisho lao baada ya kumkosa Eliaquim Mangala kutoka Manchester City.
CHELSEA KUPOTEZA £20M DILI LA COSTA
Chelsea watalazimika kukubali fedha kichele katika ofa ya Diego Costa tofauti na ile waliyotarajia wangeipata kwa biashara ya mchezaji huyo, kwa mujibu wa Sun .
Costa amekuwa tu kama mchezaji wa ziada Darajani, na tetesi zinamhusisha kuwa kwenye mchakato wa kurejea Atletico Madrid.
Lakini miamba hao wa Ligi ya Hispania wapo tayari kulipa paundi milioni 30 tu, ikiwa ni kudogo zaidi ya paundi milioni 50 walizotoa Chelsea kumsajili mshambuliaji huyo.
PSG WANATAKA £32M KWA DRAXLER
Arsenal wapo tayari kumsajili Julian Draxler, na PSG wanataka kiasi cha paundi milioni 32 kukamilisha usajili wa mchezaji huyo majira ya joto, kwa mujibu wa The Times .
YERRY MINA MBIONI KUTUA BARCELONA
Yerry Mina amekamilisha uhamisho wake kutimkia Barcelona na atajiunga na miamba hao wa La Liga akitokea Palmeiras mwakani 2018, kwa mujibu wa Sport .
TAARIFA ZAIDI ZA TETESI ZA USAJLI NA USAJILI ULIOKAMILIKA USIKOSE KUTUFUATILIA JUMATATU-IJUMAA KUPITIA DIRA YA MICHEZO, BALOHA FM 95.3-KAHAMA.

No comments
Post a Comment