Enock Atta Agyei akiwa Azam FC.
Enock Atta Agyei alianza kuonyesha
kipaji chake akiwa na umri wa miaka sita tu, akianzia kucheza katika timu ya
vijana ya King Solomon inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Ghana mwaka 2005.
Kipaji chake kikubwa cha kusakata
mpira, kilimfanya akibebe kikosi cha Shule ya Msingi Effiduase Presby aliyokuwa
akisoma, ambacho kilifuzu ngazi ya kanda na baadaye mkoa katika michuano ya
shule nchini humo.
Enock Atta Agyei akiwa Medeama fc ya Ghana.
Mara baada ya michuano hiyo, Agyei
alikuwa ni miongoni mwa nyota 26 waliochaguliwa kujiunga na Chuo cha Taifa
Michezo nchini humo, wote wakipendekezwa kuingia katika academy ya chuo hicho.
Kujitoa kwake na kufanya kazi kwa
bidii kulimfanya apandishwe haraka kutoka timu ya vijana chini ya umri wa miaka
12 hadi 17 kabla hajajiunga na Windy Professionals.
Nyota ya kinda huyo ilizidi kung’ara
mwaka jana wakati alipoichezea msimu wa mwisho Windy Professionals na hii ni
baada ya kuchangia mabao 24 yaliyofungwa na timu hiyo msimu uliopita, akifunga
mwenyewe 17 na kutoa pasi za mwisho saba ndani ya mechi 29 alizocheza.
Mafanikio yake hayo yalimfanya
azawadiwe Tuzo ya Mchezaji Bora anayetabiriwa kutikisa baadaye (GN Bank Award),
hii ikiwa ni kwa msimu 2015-2016 wa Ligi Daraja la Kwanza Ghana wakati
akiichezea Windy.
Desemba mwaka jana, haikushtua
kusikia Medeama FC ya huko ikinasa saini yake, ambayo amefanikiwa kuiongoza
kufika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kabla ya wiki iliyopita
kutua Azam FC.
Kinda huyo mbali na kutokuwa na
uzoefu wa mikikimikiki ya Ligi Kuu, tayari ameshawahi kuitwa katika timu za
Taifa za vijana za Ghana, akianzia ya chini ya miaka 17 na sasa akiwa kwenye
kile cha chini ya miaka 20.
Licha ya kutocheza hata mechi moja
mpaka sasa akiwa na U-20 ya Ghana, Agyei alikuwemo katika kikosi cha timu hiyo
kilichotolewa na Senegal kwa jumla ya mabao 3-2 kwenye mechi za kufuzu fainali
za Mataifa ya Afrika kwa Vijana wa umri huo zitakazofanyika Zambia mwakani.
Hivi sasa , Azam FC ndio
imefanikiwa kunasa saini ya Enock Atta Agyei, ambaye tayari amesaini mkataba wa
miaka miwili, huku ikimbidi kusubiri kuitumukia kalabu yake kwa kuwa
alisajiliwa akiwa chini ya umri wa miaka 18.
Huyu ndiye kinda Mghana Enock
Atta Agyei anayetoa somo kwa vijana wa
Kitanzania kuchukua hatua ya kujifunza kutokea kwake kwakuwa hakukata tamaa ya
kusubili, Leo Viongozi wa soka letu na timu zetu wanajifunza nini?.
Makocha wa timu
zetu za vijana na Timu ya Taifa ya Wakubwa wanatoa nafasi gani kwa vijana wetu
chipukizi waliopo nchini na waliopo nje ya nchi kuja kuwekeza kwenye soka letu?.


No comments
Post a Comment