Rais Abdelaziz Bouteflika wa Algeria ametoa wito kwa nchi zote duniani kushikamana kwa ajili ya kung'oa mizizi ya ugaidi.
Katika barua ya rambirambi aliyomtumia Waziri Mkuu wa Uhispani, Mariano Rajoy, Bouteflika amelaani mashambulizi ya Alkhamisi iliyopita katika mji wa Barcelona na kusema kuwa: Magaidi hawathamini uhai wa mwandamu na wanafanya kila wawezalo kuangamiza maadili na thamani za kibinadamu kama uhuru na maelewano.
Rais wa Algeria amesema nchi yake inatangaza mshikamano na Uhispania katika mapambano dhidi ya ugaidi na ameutaka tena Umoja wa Mataifa kuzihamasisha nchi mbalimbali kwa ajili ya kupambana na ugaidi na kuimarisha mazungumzo baina ya mataifa na tamaduni mbalimbali.
Watu 14 waliuawa na wengine 130 kujeruhiwa katika shambulizi la kigaidi la juzi Alkhamisi kwenye eneo la Las Ramblas mjini Barcelona, Uhispania.

Mapema jana Ijumaa pia polisi ya Uhispania iliwapiga risasi na kuwaua watu watano wanaoshukiwa kuwa magaidi. Watu hao walijaribu kugonga watu waliokuwa wakitembea kwa miguu katika eneo la Cambrils lililoko umbali wa kilomita 120 kutoka Barcelona. Polisi wanasema washukiwa hao wamejeruhi raia 6 na polisi mmoja.
Kundi la kigaidi la Daesh limetangaza kuwa ndilo lililopanga mashambulizi hayo.

No comments
Post a Comment